25 Desemba 2021 - 18:30
Mazoezi ya kijeshi ya "Mtume Mtukufu 17", ujumbe mzito, halisi na wa kivitendo kwa utawala wa Kizayuni

Mazoezi ya pamoja ya kijesi yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu (SAW) 17, yaliyoanza Jumatatu iliyopita kwenye mwambao wa Ghuba ya Uajemi, Mlango-Bahari wa Hormuz na eneo la mikoa ya Hormozgan, Bushehr na Khuzestan, yalimalizika jana Ijumaa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Iran amesema kuwa, mazoezi hayo yalipangwa mapema, hata hivyo vitisho vingi, lakini vitupu vya viongozi wa utawala wa Kizayuni, vimekuwa sababisha ya mazoezi haya kufanyika wakati huu. Amesema mazoezi haya ni miongoni mwa maneva yenye mafanikio zaidi ya makombora ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yaliyokwishafanyika hadi sasa.

Ijapokuwa vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran si jambo geni, lakini tangu kuanza kwa mazungumzo ya nyuklia ya Vienna ya kuiondolea Iran vikwazo, payukapayuka za utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran pia zimeingia katika awamu mpya. Katika wiki za karibuni, maafisa wa utawala huo haramu wamefanya harakati kubwa za kidiplomasia wakijaribu kuonyesha kuwa, shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani nchini Iran ni tishio kwa utulivu na usalama wa kikanda. Ingawa vitisho vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ni kielelezo cha vita vya kisaikolojia na harakati za propaganda za pamoja za Marekani na Israel, lakini payukapayuka hizo pia hazikupita hivihivi bila ya kupatiwa majibu. 

Kamanda wa Kamandi Kuu ya Khatam al-Anbiya (SAW) Meja Jenerali Gholam Ali Rashid amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kutoa vitisho dhidi ya vituo vya nyuklia na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya ruhusa na uungaji mkono wa Marekani na kueleza kuwa: "Iwapo vitisho hivyo vitatekelezwa kivitendo, basi Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran litashambulia vikali vituo, kambi, njia na anga iliyotumiwa kwa ajili ya hujuma hiyo."

Propaganda chafu za utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanyika licha ya kwamba, maafisa na wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) wamethibitisha mara kadhaa kwamba shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia nchini inafanyika kwa malengo ya kiraia. Ukweli ni kuwa, Israel ndiyo tishio kwa amani ya eneo la Magharibi mwa Asia kutokana na kumiliki silaha za nyuklia na harakati zake za ugaidi na uharibifu.

Katika barua yake ya hivi karibuni kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika umoja huo, Majid Takht-Ravanchi aliashiria ongezeko na ukali wa vitishio vya utawala wa Israel na kusema kuwa vitisho hivyo vimefikia viwango cha tahadhari na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, hasa Kifungu cha 2 (4) cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katika mgawanyo wa kazi na majukumu unaofanyika kwa mpangilio maalumu, maafisa wa Israel wanaonekana kujaribu kutumia vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran ili kuongeza mashinikizo ya kisiasa na kiusalama na kuathiri vibaya mchakato wa mazungumzo ya Vienna. Hata hivyo vitisho hivyo vimeonekana kutokuwa na thamani hata kwa watetezi wa Israel.

Gazeti la New York Times limeandika katika ripoti yake kwamba: Maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Israel wanaamini kuwa, utawala huo ghasibu hauwezi kuchukua hatua madhubuti za kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, kama unavyodai.

Kituo cha wanafikra wa Marekani cha The Atlantic Council pia kimesema katika uchambuzi wake kwamba: "Kutenga bajeti ya dola bilioni 1.5 kwa ajili ya jeshi la Israeli ili kujiandaa kwa shambulio la Irani utakuwa mwanzo tu wa gharama kubwa, na shambulio la kambi ya muqawama litaisababishia Israel hasara kubwa kupita kiasi."

Hata hivyo, kutokana na tabia yake ya uchokozi na kupendea kuibua migogoro, utawala wa Kizayuni unaweza kuwa na nia ya kufanya uovu na kutoa dharuba kwa mazungumzo ya Vienna. Kwa msingi huo, Jeshi la Iran limeongeza kiwango cha maandalizi na utayarifu wake ili kukabiliana na uovu huo. Ni kwa kutilia maanani hayo yote ndipo Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Hossein Salami, akasema mazoezi hayo yana ujumbe wa wazi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa, ujumbe wa mazoezi hayo ni mzito kwa utawala wa Kizayuni kwamba unapaswa kuchukua tahadhari usifanye kosa lolote, kwani ukiibua chokochoko mikono yake itakatwa.

 

342/